| Tamasha! Mbiu ya mgambo ikilia ujuwe kuna jambo. Hivyo ndivyo jamii ya Waswahili ilivyoamini tokea dahari na enzi na ukweli huo kubakia kuwa hivyo hadi hii leo. Pia ni ukweli usiokuwa na ubishi kwamba pale upepo wa kusi kama ilivyo sasa au kaskazi baadaye kabla ya mwisho wa mwaka ukipuliza ndio, jahazi, chombo kilichowaunganisha watu wa nchi kadha za Afrika, Arabuni na Asia kwa mengi, kama vile biashara, mila na utamaduni kilipotweka na kuanza safari zake. Hivi sasa safari ya aina yake ya jahazi, lakini ikiwa nchi kavu, ambayo inatarajiwa kuwakumbusha watu wa nchi hizi za majahazi kule walikotoka na utamaduni, mila na mshikamano mkubwa wa wazee wao imetweka kando kando ya ufukwe wa Bahari ya Hindi. Safari hii ni ile ambayo hivi sasa ni ya kila mwaka. Hii sio safari nyengine isipokuwa ile inayopata umaarufu mkubwa mwaka hadi mwaka... Tamasha la Utamaduni la nchi za Jahazi. Tamasha hili kwa sasa ndio kubwa kuliko lolote la aina yake katika Bara la Afrika ambalo lengo lake kuu ni kuendeleza utamaduni, mila, silka na maelewano ya watu wa nchi hizi za majahazi na kukuza vipaji vya wasanii wa nchi zinazopakana na Bara Hindi Afrika, Arabuni na Asia. Kwa kupitia Tamasha hili ambalo ni la tatu tokea kuanzishwa kwake, watu wa Zanzibar na nchi za jirani watajionea sanaa mbali mbali na kuweza kupima maendeleo yaliyopatikana katika fani hii na huku wakitafakari ni njia zipi ndio zitakazofaa ili kuendeleza utamaduni huu wa kujivunia. Jahazi ambayo ndio nembo ya tamasha limefanya kazi kubwa kwa miongo mingi mpaka hivi karibuni kutoa huduma ya usafiri kwa abiria na bidhaa katika nchi za Bara ya Hindi kwa kutegemea upepo wa kusi kama huu unaovuma sasa na wa kaskazi hapo baadaye. Ni jahazi hili ndio liliosafirisha elimu katika fani mbali mbali kutoka nchi moja kwenda nyengine, ujuzi, utamduni, mila silka na desturi na hata kuwa kichocheo cha kuanzi-shwa kwa familia za watu wenye asili ya nchi mbali mbali za Bara Hindi. Kila kitu kina chanzo na sababu zake katika maisha na unaweza kusema chanzo na sababu ya familia nyingi za Visiwani zimetokana na jahazi, mzee mmoja ambaye ni nahodha wa zamani katika safari za msimu wa majahazi, Mzee Ali Bakari (65) ambaye umaarufu wake ni Mzee Makoroma kutokana na biashara ya kuuza nazi katika soko la Chake Chake anelezea alipokuwa akikumbuka zama zake pale walipokuwa wakitweka na kufanya safari ya kati ya siku 25 hadi 30 kutoka Zanzibar hadi Arabuni. Na ni jahazi ndio liliomtoa mzee huyu wa kijiji cha Mkwajuni, Unguja, kutoka bandari ya Mkokotoni na kufanya maisha mapya kisiwani Pemba baaada ya kustaafu kazi ya baharini. Tamasha la Utamaduni la nchi za Jahazi ambalo litafanyika Zanzibar kutoka tarehe 30 Juni mpaka tarehe 10 Julai limevuitia wasanii wengi, baadhi yao maarufu sana katika filamu, michezo ya kuigiza, ngoma, maonyesho ya kazi za mikono, makongamano, muziki na mavazi. Pia patakuwepo maonyesho ya akina mama na watoto. Sasa la mgambo limelia... kuna jambo... tena kubwa Zanzibar. Asiye mwana apande jahazi kuja Visiwani kujionea mambo. Miongoni mwa shamra shamra za tamasha hili ni hizi zifuatazo:
|